KAMATI YA MAAFA KITENGO CHA OPERESHENI NA MAWASILIANO YA DHARURA YAFANYA ZIARA MRCC- TASAC

Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, Operesheni na Mawasiliano ya Dharura imetembelea Kituo cha Uratibu wa Utafutaji na Uokoaji inapotokea dharura Majini (MRCC) ambacho kipo chini ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Akieleza lengo la ziara hiyo, iliyofanyika, leo tarehe 16 Januari, 2025, katika kituo hicho kilichopo jijini Dar es Salaam, Bi. Janeth Alfred Kikunya, Mkurugenzi Msaidizi Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna mifumo ya TASAC inavyofanya kazi katika kuratibu masuala ya utafutaji na uokoaji inapotokea dharura majini.
“Ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kitengo cha Maafa Operesheni na Mawasiliano ya Dharura. Ufanisi wa kituo hiki ndio hasa chachu ya sisi kuja kutembelea na kujifunza kutoka TASAC, hususan jinsi mifumo inavyofanya kazi katika kuratibu utafutaji na uokoaji,” amesema Bi. Kikunya.
Naye Kaimu Meneja Usalama na Utunzaji Mazingira Majini Nahodha Alex Katama ameeleza namna mifumo ya kituo hicho inavyotumika kutoa taarifa na kuratibu wadau katika kushiriki zoezi la utafutaji na uokoaji pindi inapotokea dharura majini.
“Mifumo yetu ina muingiliano na wadau wa utafutaji na uoakoaji kulingana na dharura inayotokea majini na ina uwezo wa kutambua uelekeo wa chombo na mahali kilipo kiwapo safarini na kurahisisha kutoa usaidizi mara dharura inapotokea,” amesema Nahodha Katama.
Ugeni huo pia ulipata fursa ya kupata maelezo ya kina kuhusu utaratibu unaotumika kupokea taarifa zinazosaidia kuratibu zoezi la uokoaji, utoaji taarifa ya hali ya hewa majini pamoja na matumizi ya rada katika kutoa taarifa kwa mfumo wa GPS ili kusaidia kutoa uelekeo wa masafa na mawasiliano ya satelaiti kwa meli zinazofanya safari ndani na nje ya Tanzania ikiwemo “Distress” na “Navigation Warning”.
Bi. Kikunya aliambatana na Nahodha Emmanuel Lyimo (Navy) na Bi. Doroth Pantaleo. Ugeni umefurahishwa na utendaji kazi wa kituo na pia wamepongeza ufanisi wa kituo na kuongeza kuwa kituo hicho kimepiga hatua kwa kuwa na mifumo ya kisasa inayolingana na hali ya kiteknolojia nchini.