Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAWAELEKEZA WATOA HUDUMA USAFIRI MAJINI KUZINGATIA SHERIA NA KANÙNI

Imewekwa: 19 December, 2024
TASAC YAWAELEKEZA WATOA HUDUMA USAFIRI MAJINI KUZINGATIA SHERIA NA KANÙNI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa wito kwa watoa huduma ya usafiri majini kubeba abiria kwa mujibu wa leseni ya chombo kilichopewa.

Hayo yamesemwa na Mkaguzi Mwandamizi wa TASAC, Mhandisi Rashid Katonga, leo tarehe 17 Desemba,2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa ukaguzi wa boti zinazotoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Mhandisi Katonga amesema kuwa TASAC hufanya shughuli za ukaguzi wa vyombo ili kuona kama vinatimiza masharti ya leseni zao na kutaja kuwa kaguzi za kushtukiza zinafanywa kuona kama watoa huduma wanazingatia kanuni na taratibu za usalama wa usafiri majini.

"Tupo hapa kukagua  na kuona abiria waliokatiwa tiketi  na kusafirishwa ni sawa na uwezo wa chombo cha usafiri majini kwani tunafahamu  huu ni msimu wa sikukuu hivyo wasafiri uwa ni wengi, hivyo, mahitaji ya usafiri uongezeka sana,” amesema Mhandisi Katonga.

Ameongeza kuwa ni takwa la kisheria kwa watoa huduma wote nchini wa usafiri majini kutoa huduma kwa kufuata masharti ya leseni, kanuni za usalama na matumizi ya vifaa okozi hasa katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuuu za mwisho na mwanzo wa mwaka ambapo wasafiri wamekua wengi zaidi.

Naye Mwakilishi wa Kampuni ya Azam, Naho. Feruzi Kassim ameipongeza TASAC kwa kufanya kaguzi hizo ili kuwakumbusha watoa huduma kuwa makini na kutimiza matakwa ya sheria katika kuendesha vyombo vya usafiri majini.

“TASAC wako makini na kazi yao na wanajua majira yenye vishawishi vya kuvunja masharti ya leseni ila sisi nasi tunatekeleza matakwa ya leseni  na kanuni za usalama wa usafiri majini ili kuhakikisha usalama wa abiria wetu pamoja na mizigo. Ni jambo jema wote tushirikiane  kuhakikisha usafiri huu unaendelea kuwa salama," amesema Naho. Kassim.

Zoezi la ukaguzi wa usalama wa usafiri majini ni endelevu kwa nchi nzima. TASAC ulitilia mkazo sana hasa katika majira ya sikukuu za mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka ambapo watu wengi usafiri kwa minajili mbalimbali.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo