WADAU WA ULINZI NA USALAMA WA BANDARI WAASWA KUSHIRIKIANA

Wadau wa masuala ya ulinzi wa bandari na usalama wa uendeshaji vyombo baharini wameaswa kushirikiana na kupeana taarifa katika utekeleaji wa masuala ulinzi, usalama na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Ulinzi wa bandari na Usalama wa Uendeshaji vyombo Bahari (Port Security and Safety to Navigation), leo tarehe 6 Februari 2025, Afisa Mfawidhi wa Kamisheni ya Ukanda wa Magharibi ya Bahari ya Hindi (Indian Ocean Commission), Bw. Raj Mohabeer amesema kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa mradi hususani katika kubadilishana taarifa baina ya wadau na hivyo kupelekea ugumu katika utekelezaji wa masuala ya Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira.
“Kitu nilichojifunza ni uwepo wa changamoto ya kubadilishana taarifa baina ya wadau wa masuala ya ulinzi na usalama katika nchi husika, mfano Wizara ya Uvuvi inatoa leseni kwa vyombo vya uvuvi lakini inapotokea kuna chombo kinafanya shughuli za uvuvi na hakina leseni wanaohusika kukamata Chombo ni Polisi wanamaji na taarifa za vyombo vilivyosajiliwa zipo Wizara ya Uvuvi peke yake,” amesema.
Aidha ameongeza kuwa changamoto za kiusalama zinazotokea baharini kwa nchi ya Tanzania zinaweza kuathiri nchi nyingine za jirani na hivyo kutoa wito kwa nchi wanufaika wa mradi kushirikiana.
Kwa upande wake Nah. King Chiragi ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TASAC amesema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuangalia namna gani Ukanda wa Magharibi ya Bahari ya Hindi unaweza kufikia malengo ya usalama wa bandari na safari za meli katika maeneo ya ukanda huo.
“Bahari imeungana kinachofanyika kwetu kinaweza kuathiri sehemu nyingine na kinachofanyika nchi nyingine kinaweza kuathiri ufanisi wetu wa bandari pamoja na Uchumi wetu, hivyo ni lazima tuangalie namna nzuri ya kutunza mazingira ya bahari kwa kushirikiana,” amesema Naho. Chiragi.
Kwa upande wake, Stella Katondo, Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira Wizara ya Uchukuzi ameeleza jinsi Tanzania ilivyonufaika na mradi wa wa Ulinzi wa Bandari na Usalama wa Uendeshaji vyombo Bahari (Port Security and Safety to Navigation) ikiwemo kuongeza idadi ya kaguzi za meli pamoja na Uwezeshaji wa taasisi zinazohusia na utekelezaji wa masuala ya ulinzi, usalama na utunzaji wa mazingira baharini (Capacity building).