WADAU WATOA MAONI KUTATUA CHANGAMOTO SEKTA YA USAFIRI MAJINI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 03 Desemba, 2024, limekutana na wadau wa usafiri majini katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Utalii Dar es Salaam na kupokea maoni ya namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika sekta hiyo.
Akifungua Kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara za Meli, Bw. Nelson Mlali amesema kuwa moja ya jukumu la Shirika ni pamoja na kutoa fursa kwa wadau kuwasilisha maoni na kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kukutana ni kuboresha huduma katika sekta ya usafiri majini, kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zinazoibuliwa pamoja na kutoa ufumbuzi wa malalamiko yanayojitokeza katika sekta hiyo.
"Suala la kupokea maoni yanayotokana na changamoto mnazokutana nazo ni jambo muhimu kwa ajili ya kukuza sekta ya usafiri majini na kuboresha huduma zinazotolewa ili ziwe zenye viwango vya juu," amesema Bw. Mlali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri Majini TASAC, Bw. Julius Mitinje amesema suala la kupokea maoni yanayotokana na changamoto wanazokutana nazo wadau katika sekta usafiri majini ili kuboresha huduma za usafiri majini.
Kikao kilipokea maoni ya wadau kuhusu mapendekezo yanayotokana na changamoto wanazokabiliana nazo ili kuboresha utendaji katika sekta hii na namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.
Kikao hicho kiliwahusisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Bandari (TPA), Makampuni ya Utoaji wa Huduma Ndogo Bandarini (Miscellaneous Port Services), Makampuni ya Uwakala wa Meli (Shipping Agents) na Makampuni ya Kuhakiki Shehena (Ship Tallying).