Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

Wadau watoa maoni mabadiliko ya kanuni za kushughulikia Malalamiko

Imewekwa: 13 August, 2024
Wadau watoa maoni mabadiliko ya kanuni za kushughulikia Malalamiko

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limekutana na wadau wa usafiri majini katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Utalii Dar es Salaam na kupokea maoni juu ya mabadiliko ya kanuni za kushughulikia malalamiko ya mwaka 2018.

Kikao hicho, kilichofanyika tarehe 12 Agosti, 2024,  kilifunguliwa na Mkurugenzi wa Huduma za Usafirishaji wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Biseko Chiganga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi.

Bw. Chiganga alisema kuwa ni takwa la kisheria kuwapa fursa wadau kutoa maoni kila kanuni zinapotungwa au kubadilishwa ili kusaidia kuziba mianya ya utatuzi wa malalamiko yanayojitokeza katika sekta ya uchukuzi majini.

"Suala la kutatua malalamiko  ya wateja katika sekta ya usafiri majini ni jambo muhimu kwa ajili kukuza sekta usafiri majini na kuboresha huduma kwa wateja," alisema Bw. Chiganga.

Kikao kilipokea maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni ili kuboresha mfumo wa kushughulikia malalamiko yanayowasilishwa TASAC dhidi ya watoa huduma inaowadhibiti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Biashara za Meli TASAC, Bw. Nelson Mlali ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, alisema suala la kutatua malalamiko katika sekta usafiri majini ni muhimu na ni endelevu kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri majini.

Amesema kuwa malalamiko ya wateja yanaweza kutokea kutokana na kuvunjwa kwa mikataba, utoaji huduma yenye viwango duni, tozo au utaratibu mbovu wa kushughulikia malalamiko.

“Mabadiliko yanakuja kwa sababu mazingira ya utoaji huduma ya uchukuzi yanabadilika na kuhitaji maboresho,” aliongeza.
Wadau mbalimbali wakiwemo Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA), Mawakala wa Meli (TASAA), na Baraza la Wasafirishaji wanaendelea kutoa maoni ili kuboresha kanuni hizo.

Wadau wanaweza kuwasilisha maoni yao kwenda  TASAC kwa njia ya maandishi ndani ya muda wa siku 14 kuanzia tarehe 12 Agosti, 2024 kupitia barua pepe dg@tasac.go.tz.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo