WADAU WATOA MAONI MAPITIO YA TOZO ZA UTOAJI MIZIGO BANDARINI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 06 Februari, 2025, limekutana na wadau wa usafiri majini na kupokea maoni ya tozo za utoaji mizigo, katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema kuwa Shirika lina wajibu wa kutoa fursa kwa wadau kuwasilisha maoni na kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku. Hivyo, Shirika limetoa mwanya kwa wadau kutoa maoni katika mapitio ya tozo za utoaji mizigo bandarini.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kukutana ni kuboresha huduma katika sekta ya usafiri majini, kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zinazoibuliwa pamoja na kutoa ufumbuzi wa malalamiko yanayojitokeza katika sekta hiyo.
“Mkutano huu ni sehemu ya mchakato wa upokeaji maoni ambao utampa nafasi kila mdau kutoa maoni yake ili kuboresha sekta ya usafiri majinii. Nataka niwahakikishie kuwa mkutano huu unafanyika kwa uwazi ili kuwapa washiriki fursa sawa za kutoa maoni na uzoefu wao husika ili kuwezesha kufanya maamuzi yenye tija kwa Sekta ya Usafiri Majini na Taifa kwa ujumla,” amesema.
Ameongeza kuwa maoni yote yatakayotolewa wakati wa mkutano huo yatachukuliwa na kuzingatiwa ipasavyo katika kufanya maamuzi ya mwisho. Na alitumia fursa hiyo kuwaomba wadau kushirikiana na TASAC ili kuhakikisha kuwa mchakato wa utoaji maoni unaleta matokeo chanya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi TASAC, Bw. Nahson Sigalla amesema kuwa mchakato wa kukusanya maoni utaendelea kwa siku saba zaidi ili wadau wengi zaidi wapate nafasi ya kutoa maoni.
Kikao hicho kiliwahusisha wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya Bandari (TPA), Makampuni ya Utoaji wa Huduma Ndogo Bandarini (Miscellaneous Port Services), Makampuni ya Uwakala wa Meli (Shipping Agents), Makampuni ya Mawakala wa forodha (Clearing and Fording Agents) na Makampuni ya Kuhakiki Shehena (Ship Tallying).