Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

MNYORORO WA UGOMBOAJI BIDHAA ZA KIPEKEE WAPIGWA MSASA

Imewekwa: 24 May, 2024
MNYORORO WA UGOMBOAJI BIDHAA ZA KIPEKEE WAPIGWA MSASA

 

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 23 Mei, 2024 katika jengo la SUMTRA jijini Dar es Salaam limekutana na wadau wanaohusika katika mnyororo wa ugomboaji wa bidhaaa za kipekee na kujadiliana namna ya kuboresha uharakishaji wa mnyororo wa ugomboaji wa bidhaa za kipekee unaofanywa na TASAC.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Nelson Mlali ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Biashara za Meli TASAC amefungua kikao hicho kwa kuwashukuru wadau hao kukubali kuhudhuria kikao hicho kinacholenga kujenga uelewa wa shughuli zinazofanywa na TASAC lakini pia kuboresha mahusiano.

"Kikao hiki kinatuunganisha, tunabadilishana uzoefu, tunajengeana uwezo wa uelewa wa shughuli zinazofanywa na TASAC hasa katika jukumu hili la kugomboa bidhaa za kipekee, tunaboresha mawasiliano miongoni mwetu na kutatua changamoto katika mnyororo wa ugomboaji". Amesema Bw. Mlali.

TASAC ina jukumu la kugomboa bidhaa za kipekee ambazo ni makinikia, siraha na vilipuzi, kemikali zinazotumika kwenye migodi ya madini, nyara za serikali  na wanyama hai kwa mujibu Sheria ya Wanyama Mapori Sura 283. 

"Majukumu ya kipekee yanafanywa na TASAC pekee na hakuna wakala wa forodha anapaswa kufanywa. Wigo wa bidhaa hizi ulipunguzwa tangu pale mabadiliko ya Sheria ya fedha Na.5 ya mwaka 2022 ilipoondoa baadhi ya bidhaa.
Mnyororo  huu ukiharakisha unasaidia kuongeza wateja wanaotumia bandari ya Dar es Salaam na kuongeza kipato kwawadau na Serikali kwa ujumla." Ameongeza Bw. Mlali

Katika kikao hicho, mawasilisho mawili yamewasilishwa ambayo ni kufahamu Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania na wigo wa majukumu kugomboa bidhaa za kipekee; na taratibu za ugomboaji wa mizigo ya kipekee.

Aidha, wadau walipata fursa ya kujadiliana na kuona kuwa upo umuhimu mkubwa wa TASAC pamoja na wadau kuwa na mawasiliano ya karibu ili kuharakisha utoaji wa bidhaa hizo zinafuata taratibu zote za nchi na kutatua changamoto yoyote ya ukwamishaji endapo itatokea.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Polisi, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA).

Mrejesho, Malalamiko au Wazo