Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ametoa rai kwa watoto wa kike kujiunga na fani ya Ubaharia

Imewekwa: 07 October, 2023
Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ametoa rai kwa watoto wa kike kujiunga na fani ya Ubaharia

Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa ametoa rai kwa watoto wa kike kujiunga na fani ya Ubaharia  ili kuongeza idadi kubwa ya wataalamu wa jinsia ya kike katika sekta ya Usafiri kwa njia ya maji.

Akizungumza hayo katika ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Bahari 2023  uliofanyika katika Viwanja vya Gombani Nje Visiwani Pemba - Zanzibar tarehe 25 Septemba, 2023 Mhe. Mbarawa amesema kuwa idadi kubwa ya Mabaharia ni vijana wa kiume hivyo amewasihi watoto wa kike kujiunga kwa wingi katika fani ya Ubaharia kwani ni fani nzuri na yenye manufaa.

"Fani ya Ubaharia sio ngumu kama ambavyo baadhi ya watu wanadhani, pia sio fani kwa ajili ya vijana wa kiume pekee bali ni fani ya jinsia zote mbili, hivyo vijana wakike ni wakati wenu sasa kukimbilia fursa hii ili kujiinua kiuchumi lakini pia kwa maendeleo ya Taifa letu kwa ujumla". Amesema Mhe. Mbarawa.

Aidha, Mhe. Mbarawa amewasihi mabaharia wote na wavuvi kuendelea kuchapa kazi kwa weledi huku wakichukua hatua za kulinda mazingira ya bahari, maziwa na mito.

Pia, Mhe. Mbarawa amewapongeza kamati kwa kufanikisha maandalizi ya maadhimisho hayo lakini pia kwa washiriki wote waliohudhuria.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bw. Nelson Mlali ametoa wito kwa wananchi wote wanaotumia vyombo vya usafiri majini kujenga utamaduni wa kutunza mazingira muda wote wawapo safarini.

"Naomba nitoe wito kwa wananchi wote wanaotumia vyombo vya usafiri majini kujenga utamaduni wa kutunza mazingira kipindi chote muwapo safarini au katika shughuli nyinginezo ili kunusuru mazingira ya bahari". Amesema Bw. Mlali.

Maandimisho ya Siku ya Bahari Duniani 2023 yenye Kauli mbiu "Miaka 50 ya MARPOL, Uwajibikaji wetu Unaendelea" yameanza leo tarehe 25 Septemba, 2023 na yanatarajia kuhutimishwa tarehe 28 Septemba, 2023.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo